Thursday, October 20, 2016

Dk Slaa Aingilia Kati Ugomvi wa Godbless Lema na RC Gambo


Ugomvi wa maneno kati ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema limemuibua katibu Mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa aliyeandika ujumbe mrefu akimkingia kifua mbunge huyo.


Gambo na Lema walirushiana maneno juzi mbele ya wafadhili kwenye hafla ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maendeleo wa ujenzi wa hospitali itakayohudumia bure wanawake na watoto uliogharimu shilingi bilioni 9.

Kupitia ujumbe huo uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ambao alithibitisha kuwa ni wa kwake, Dk Slaa amemrushia lawama Mkuu huyo wa Mkoa akidai kuwa anaijua vizuri historia ya ardhi na mradi huo.

==> Usome Hapo Chini

Mrisho Gambo,
Naamini hii ID ni ya kwako na hasa kwakuwa kwenye post unaonekana ukizungumza, napata uhakika kuwa ni wewe.

1) Mkuu wa Mkoa, nakuheshimu kwa kuwa cheo chako ni kikubwa sana. Hata hivyo, ulichokifanya leo na " propaganda unazopiga zimenifanya nikudharau na kukupuuza. Ningeliweza kuishia katika kukudharau na kukupuuza, lakini

2) Aibu uliyoiletea Taifa letu leo, inanifanya " nipige kelele" kuwa " siasa za maji taka siyo wakati wake huu.

a). Mhe.Mrisho Gambo, wewe kama Mkuu wa Mkoa unayo au mamlaka au vyombo vya dola kukusaidia kufanya utafiti wa maana kuliko aibu kubwa uliyoiletea Taifa letu mbele ya Wahisani/ Wafadhili wetu kupitia Maternity Africa. Hukufanya hivyo, umeamini propaganda kuliko busara na hekima. Kwa hilo siwezi kukusamehe wala kukuheshimu pamoja na cheo au vyeo vyote ulivyonavyo.

b). Mrisho Gambo, ungelikuwa wa busara iwapo ungelimwomba kiongozi au mwakilishi wa ADF (ulikuwa na uwezo wa kujua ADF ni nani na historiaya yake ni ipi- kwa kupenda propaganda hukufanya hivyo) au Mwakilishi wa Maternity Africa hasa Happy (ambaye alisaini pia barua ya kukualika kuwa mgeni rasmi, au hata Mhe.Mbunge Lema ambaye kimsingi ndiye chimbuko la upatikanaji wa Ardhi hiyo kutoka kwa Marehemu Advocate Mawala (Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi), na pia chimbuko la Upatikanaji mradi kutoka kwa wafadhili wetu.

Kutokupenda kushauriwa na hao wenye kujua mradi imekufanya "kuonekana juha" na " mwongo" kwa kuwa historia haifutwi kwa " propaganda za jukwaani". Lakini kwa bahati mbaya athari ya propaganda imeenda mpaka kuichafua Taifa letu kwa wahisani. Ujenzi ndiyo kwanza unaanza. Umeombwa kufanya "Ground Breaking ceremony", unadhani wawakilishi wa wahisani na hasa kule kwenye chimbuko la fedha wanapata picha gani ya Taifa letu.

c). Mrisho Gambo, busara na hekima ya kawaida ingelikuwezesha kuelewa barua ya mwaliko ambayo imesisitiza mara mbili hivi, kuwa wahusika ni taasisi isiyojihusisha na siasa. Wakasema mradi kwa muda sasa umekumbwa na matatizo yenye sura ya kisiasa. Ulipaswa kutafakari, kutafiti na kutafiti njia makini zaidi ya kuona wakina mama wajawazito, wenye fistula na watoto wachanga hawakosei au hata hawacheleweshewi kupata huduma hiyo kwa sababu za kipuuzi tu. Eti unasoma historia! Unaijua historia au unaota ndoto!

Nimepiga kelele kwa kuwa ninaijua vizuri hiyo historia A to Z. Sikuambii ungeliniuliza, lakini wapo kwenye kikao hicho ambao wasingelihitaji kuisoma bali kuitoa kichwani historia hiyo, tangu kupatikana kwa Ardhi, mchakato wa kuchora ramani, kuisajili na kupata vibali vyote vya Kituo hicho cha Afya (japo kwa kweli ni hospitali, inaitwa kituo cha Afya tu kwa. Sababu za kisheria).

3) Mrisho Gambo, kwa hili Watanzania wa Arusha na wote wenye kujua ukweli hatutakusamehe kwa aibu uliyotupatia, na kujenga misingi ya kutufungia miradi mingine kwa wahisani wetu.

Kama una chembe dogo la busara:
a). Utakaa chini na kutafakari umekosea wapi.

b). Uwe na unyenyekevu uwaite wahusika wote ofisini kwako waombe wakupe " historia kamili" na wakupe mchakato mzima mpaka kufikia siku hii muhimu ya "Ground Breaking ceremony (uzinduzi wa Kazi ya ujenzi).

c). Ukipata Taarifa kamili, uwe na unyenyekevu, acha kiburi. Kiburi hakikusaidii wala haitasaidia jamii unayopaswa kuwatumikia (unless una malengo tofauti). Kwa unyenyekevu mkubwa Waombe msamaha Wahisani wetu kwa kuwaingiza katika " siasa ya Arusha" ambayo hawahusiki nayo; awaombe msamaha wakina mama, watoto na jamii ya Wananchi wa Arusha wapenda maendeleo kwa kuwachafua na kuwaletea vurugu kiasi cha kuifanya Arusha ionekane kila leo ni mahali pa vurugu, kumbuka vurugu husababishwa na viongozi wasiotumia busara na hekima. Uongozi ni busara na hekima siyo mabavu wala nguvu ya mamlaka.

Nimeyasema haya kwa uchungu mkubwa. Mimi siko kwenye siasa, na wala sina interest na siasa. Siangalii uso wa mtu. Kama ambavyo niliaga kuwa " Nastaafu Party Politics, lakini nitapiga kelele pale maslahi ya Taifa langu yanavyokanyagwa" nitakuwa mwendawazimu kunyamaza wakati mradi wa Tshs Takriban 9 Billioni unahatarishwa na upuuzi na uzembe wa kiongozi mmoja mwenye kuendekeza propaganda zisizo na msingi.

Nawaomba sana Radhi wahisani wetu. Mtuvumilie siyo kwa ajili yetu bali kwa ajili ya kina mama na watoto walengwa wa huduma itakayotolewa na " Kituo cha Mama na Mtoto" (propaganda kwamba Hospitali ni ya mke wa Lema zipuuzeni).

Happy, umevumilia mengi katika miradi mingi uliyofadhili na kuisimamia. Usirudi nyuma. Timiza ndoto yako iliyoanza katika umri mdogo sana. Matunda yanaonekana pamoja na vikwazo vya mara kwa mara vya wapinga maendeleo. Viongozi, " Tenganisheni siasa na Maendeleo" Watumikieni Watanzania bila kuangalia nyuso zao, mrengo wao. Siasa ni sayansi na siasa ni utumishi.

Dr.Wilbroad Peter Slaa
Share:

Dully Sykes kuja kivingine na tour ya Dar ‘kwa mara ya kwanza nitakuwa na Mabaunsa’


Msanii wa muziki anayefanya vizuri na wimbo ‘Inde’ Prince Dully Sykes amejipanga kuja kivingine katika tour yake jijini Dar es salaam ambayo itaanza weekend hii Club 71.

Akiongea na Bongo5 Alhamisi hii, Dully amesema ameamua kufanya baadhi ya mabadiliko kwenye team yake ili kuonyesha utofauti wa Dully wazamani na huyu wa sasa.

“Mikoani mambo yalikuwa mazuri sana namshukuru Mungu na sasa ni zamu ya Dar es salaam,” alisema Dully “Tour yangu ya Dar itaanzia Club 71. Kutakuwa na surprise zakutosha, pia Dully nitakuja kivingine nikiwana na mabaunsa, kwa sababu huyu pia ni Dully mpya ambaye anahitaji usalama kwenye show zake,” Muimbaji huyo amesema katika show hiyo atasindikizwa na wasanii ambao atawaweka wazi hapo baadae
Share:

Beny Kinyaiya Afungukia Ishu Ya Ushoga

Mtu Kati: Vipi katika kupigapiga ‘gemu za nje’, umewahi kupata mtoto au watoto?

Kinyaiya: Yaah! Nina watoto wawili, wa kwanza anaitwa Ben Kinyaiya Junior, ana miaka minne na nusu na wa pili anaitwa Nilla, huyu ni wa kike na ana miaka mitatu.

Mtu kati: Kwa muda mrefu kumekuwa na madai ambayo hayajathibitishwa kwamba unajihusisha na mapenzi ya jinsia moja (ushoga), unalizungumziaje hili?

Kinyaiya: Ni mawazo yao tu, kwanza nikwambie mimi huwa siabudu majungu. Watu walianza kunizungumzia vibaya kitambo wakinihusisha na hayo mambo, wengine wakawa wanasema eti hawajawahi kuniona na mwanamke, nikawapuuzia tu. Baadaye kibao kikageuka, wakaanza kuniita eti mimi ni malaya kwa sababu nina wanawake wengi, pia sikuwajali. Nikaendelea na maisha yangu na sasa hivi ndiyo kama hivyo tena, tayari nina watoto wawili, waliokuwa wakinizushia mambo mabaya wote wamenyamaza kimya.

Mi nafanya shughuli zangu za kimaendeleo, sina haja ya kujibizana na watu wanaozusha maneno ya uongo juu yangu, kama mtu anahisi mimi nina matatizo yoyote basi aniunganishe na dada yake atampa majibu (anacheka).
Share:

Kamati ya Bunge Yakataa faini ya 500,000/- Kwa Kila Kosa Barabarani

Kamati  ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala imekataa mapendekezo ya kufanyia marekebisho Sheria ya Leseni za Uchukuzi ya mwaka 1973 yenye lengo la kuongeza kiwango cha adhabu ya faini hadi kufikia asilimia 500 kwa watakaokiuka masharti ya leseni hizo.

Mapendekezo hayo yaliwasilishwa mbele ya kamati hiyo mjini Dodoma jana na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra).

Baada ya kuyakataa mapendekezo hayo, kamati hiyo imetoa muda wa siku mbili kwa Sumatra kuhakikisha inawasilisha mbele ya kamati hiyo mapendekezo yanayokubalika.

Sumatra inapendekeza kuongeza kiwango cha adhabu ya faini kutoka kati ya Sh 10,000 na Sh 50,000 hadi Sh 200,000 na 500,000 kwa watoa huduma za uchukuzi, watakaokiuka masharti ya leseni zao.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohammed Mchengerwa alisema mapendekezo hayo, yatazidi kuwaongezea mzigo Watanzania badala ya kuwasaidia. 
Alisema kiwango hicho cha faini kubwa, kamwe hakitazuia tatizo la ajali za barabarani, zaidi ya kuongeza ukubwa wa tatizo la rushwa.

“Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuwasaidia wananchi, lakini mapendekezo haya yatazidi kuwaongezea mzigo kwa sababu kiwango cha faini hizi kama kitapitishwa, watoa huduma za uchukuzi watahamishia hasara yao kwa wananchi,” alisisitiza.

Aliitaka mamlaka hiyo, kwenda kuyafanyia kazi tena mapendekezo hayo kwa kuwasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuwasilisha viwango vya faini vinavyokubalika. 
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Joseph Mhagama ambaye pia ni mbunge wa Madaba, alisema mapendekezo hayo hayana nyongeza yoyote, itakayoisaidia serikali katika kudhibiti tatizo la ajali barabarani.

“Kwa sasa serikali imeweka nguvu zake katika kupunguza ajali za barabarani, lakini kiwango cha faini hizi hakina uhusiano wowote na jitihada hizi zaidi ya kuiongezea Sumatra mapato na kuwapa mzigo walipa kodi,” alisema.

Akiwasilisha mapendekezo ya mamlaka hiyo mbele ya Kamati hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo, yamelenga  kuiboresha zaidi sheria hiyo ya leseni za uchukuzi.

Alisema marekebisho hayo, pia yatasaidia mamlaka hizo kuendana na mahitaji ya sasa hasa katika eneo la adhabu ya faini, hali itakayopunguza kiwango kikubwa cha kukiukwa kwa masharti ya leseni hizo za uchukuzi.
Share:

Wawili mbaroni kwa wizi wa miundombinu ya TANESCO Yenye Thamani ya Milioni 61

Wakazi wawili wa Manispaa ya Kinondoni wanashikiliwa na Polisi wakituhumiwa kukutwa na miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) yenye thamani ya Sh milioni 61.

Walikutwa na miundombinu ya shirika hilo ikiwemo vifaa kwa ajili ya kuunganishia umeme.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi saa 10 jioni katika maeneo tofauti ya manispaa hiyo.

Alisema katika tukio la kwanza, maeneo ya Makumbusho, polisi wakishirikiana na kikosi kazi cha kuzuia uharibifu wa miundombinu ya Tanesco, walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu kuwepo kwa watu wanaohujumu miundombinu ya shirika hilo.

“Kikosi kazi walifika eneo hilo katika nyumba ya Wilfred Baruti (45) mkazi wa Makumbusho na kufanya upekuzi katika nyumba hiyo na vilipatikana vifaa mbalimbali vinavyotumika kuunganisha umeme vya Tanesco,” alisema Mkondya.

Aidha, alisema pia polisi walikwenda katika nyumba nyingine ya Beatrice Emmanuel (42) mkazi wa Salasala Mabanda Mengi walikofanya upekuzi na kufanikiwa kukamata vifaa ambavyo ni nyaya aina ya drums mbili, rola ya nyaya aina ya AICC ya umeme wa milimeta 50 ambazo hutumiwa na Tanesco kituo cha Kilimahewa cha Kawe, wilayani Kinondoni.

Alisema upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani.
Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Leila Muhaji akizungumza na waandishi wa kuhusu wizi huo wa vifaa vya umeme vyenye thamani ya milioni 61,Kulia ni Kaimu Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,Lucas Mkondya.
Share:

Jeshi la Polisi Dar laua majambazi Hatari 6


Watu sita wanaotuhumiwa kuwa majambazi hatari, wameuawa katika majibizano ya risasi na Polisi katika eneo la Mbezi kwa Yusuf Makondeni katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Kanda Maalumu, Naibu Kamishna wa Polisi, Lucas Mkondya, watuhumiwa hao waliuawa katika majibizano ya risasi na Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ujambazi wa Kutumia Silaha.

Mkondya alisema wamepata taarifa kutoka kwa raia mwema kuwa kuna kikundi cha watu wenye silaha, wamejipanga kufanya tukio la ujambazi kwa kutumia silaha kwa mfanyabiashara aliyekuwa akitoka Benki ya Diamond Trust Bank (DTB), tawi la Barabara ya Nyerere, ambaye angepita katika barabara hiyo kwenda mkoani Morogoro.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo, polisi waliweka mtego na majambazi hao wakitumia gari aina ya Toyota Carina lenye namba za usajili T970 DGZ rangi ya fedha, walionekana wakilifukuza gari la mfanyabiashara huyo, kisha kulipita na kumsimamisha kwa nguvu.

“Majambazi wawili wakiwa na bastola walishuka katika gari hilo. Baada ya kugundua kuwa wameingia kwenye mtego wa polisi, walianza kufyatua risasi kwa askari wakitumia bastola na wenzao waliokuwa wamejaa kwenye gari yao walianza kushuka huku wakifyatua risasi kuelekea kwa askari,” alisema Kaimu Kamanda Mkondya.

Alisema kutokana na hali hiyo, askari walianza kujibu mashambulizi na kuwaua majambazi hao na baada ya upekuzi, zilipatikana bastola mbili, moja ya kijeshi aina ya Chinese ikiwa na risasi moja ndani ya kasha la risasi; na nyingine aina ya Browning ikiwa imefutwa namba zake na maganda sita ya risasi yaliyookotwa katika eneo la tukio.

Miili ya watuhumiwa hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na upelelezi unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa ujambazi.

Katika tukio lingine la Oktoba 17, mwaka huu saa 2:00 usiku katika maeneo ya Tegeta Masaiti, watuhumiwa watatu wa ujambazi wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki aina ya Fekon yenye namba MC370 BEY, wakiwa na bunduki aina ya shotgun iliyokatwa mtutu na kitako, walivamia duka la Abdallah Juma (46), mkazi wa Tegeta na kupora fedha za mauzo na kuiba vocha za mitandao mbalimbali, ambazo thamani yake haijafahamika.

“Polisi baada ya kupata taarifa waliwafukuza majambazi hao, walipoona wanakaribiwa na askari, walitupa chini begi walilokuwa nalo na kutelekeza pikipiki yao kisha kukimbia, begi lilipopekuliwa lilipatikana na silaha hiyo,” alisema.

Aidha, wananchi wenye hasira waliendelea kuwakimbiza majambazi hao na kumuua mmoja huku wengine wakikimbilia kusikojulikana. 

Katika hatua nyingine, Mkondya alisema wamekamata watuhumiwa wawili wa unyang’anyi kwa kutumia nguvu wakiwa na pikipiki moja na funguo bandia 75.

Alisema watuhumiwa hao, Ally Makwega (53) mkazi wa Tandika na Fabian Greyson (39) mkazi wa Yombo walikamatwa Oktoba 4, mwaka huu saa 6:00 usiku.

Watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na pikipiki yenye namba MC292 AMD aina ya Boxer rangi nyekundu, wanayoitumia kufanya uhalifu, wakiwa na funguo bandia 75 ambazo huzitumia katika kuvunja nyumba mbalimbali ya biashara za kulala wageni, maghala ya kuhifadhia bidhaa na maduka.

Baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa, walikiri kuhusika na matukio mbalimbali ya uvunjaji wa maghala na kuiba katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.

Watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Share:

Sunday, July 3, 2016

Mwigulu Nchemba Aahidi Makubwa kwa Askari Jeshi la Polisi


WAZIRI wa mambo ya ndani ya nchi Mwigulu Nchemba, amesema kuwa Serikali itahakikisha inakabiliana kwa nguvu zote na tatizo la makazi ya askari polisi nchini ili kulipa hadhi jeshi hilo ambalo linakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Nchemba aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na maafisa wa jeshi hilo pamoja na askari wa kawaida wa mkoa wa Dodoma katika kikao kazi kilichofanyika kwenye bwalo la jeshi hilo mjini Dodoma.
 
Mwigulu alisema kuwa mojawapo ya suala ambalo wizara yake italipa kipaumbele ni makazi ya askari wa jeshi hilo ambayo mengi hivi sasa yamechoka na kukosa hadhi ya kutumiwa na askari wa jeshi hilo.
 
“Suala la makazi tutalipa kipaumbele kikubwa sana na tutaanza hatua kwa hatua kulifanyia kazi suala hili ili askari wetu waondokana na adha hii wanayoipata kwa muda mrefu sasa,” alisema Mwigulu.
 
Alisema kero nyingine watakayoifanyia kazi ni kuhakikisha kuwa mazingira ya kufanyia kazi kwa askari polisi yanaboreshwa kuanzia kazini kwao na pia kwenye makazi yao.
 
“Kumekuwapo na tatizo la mafuta kwa jili ya magari mnayoyatumia … hata tukio likitokea mnashindwa kufika kwa kukosa mafuta. 
 
"Pia kuna maslahi duni, umeme maofisini pamoja na nyumbani mnapoishi imekuwa ni kero kubwa kwenu hivyo sisi kama wizara tutahakikisha haya yote tunayaondoa,” alisema Mwigulu.
 
Katika hatua nyingine, Mwigulu alitoa rai kwa askari polisi nchini kuhakikisha kuwa wanazingatia miiko ya kazi yao kwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili kama ambavyo walivyofundishwa katika mafunzo yao.
 
“Mimi uwepo wangu hapa sijaja kuwafundisha kazi kwakuwa tayari kazi yenu mnaijua… ambayo mmefundishwa mkiwa chuoni. Hivyo sisi kama wizara jukumu letu ni kuweka mazingira wezeshi ili mfanye kazi zenu katika mazingira mazuri,” alisema.
 
Aidha alilitaka jeshi hilo kutumia nguvu katika mahali panastahili tu kufanya hivyo ili hata mwanachi akisikia utendaji wao ajivunie uwapo wa jeshi hilo.
 
“Tumieni nguvu mahali mbapo Mtanzania wa kawaida akisikia ajivunie uwapo wenu kama ambavyo mmejitahidi katika suala la madawa ya kulevya. Kama tutaweza kuubaini mnyororo huo na kuukata, mwanchi wa kawaida atajivunia,” alisema.
 
Aidha alisema kuwa jeshi hilo bado lina kazi kubwa ya kufanya ili kukomesha mtandao wa watu wanaojihusisha na madawa ya kulevya nchini na pia akalitaka jeshi hilo kuhakikisha linakuwa mtetezi wa wanyonge.
 
Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, awali akimkaribisha Waziri Mwigulu alisema kuwa jeshi hilo limejipanga vilivyo katika kuhakisha uhalifu unakomeshwa mkoani hapa.
 
“Mweshimiwa waziri mwenye utakuwa ni shahidi ukiwa katika vikao vya bunge uliona namna ambavyo amani na usalama ulikuwepo wa kutosha. Hii yote ni kutokana na kujipanga vizuri kwa jeshi la polisi mkoani hapa,” alisema Mambosasa.
Share:

Rais Magufuli Atuma salamu za Rambirambi Ajali Morogoro Iliyoua Watu 12


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amezitumia salamu za pole familia, ndugu, jamaa na marafiki wa watu 12 waliopoteza maisha kufuatia ajali mbili zilizotokea katika eneo moja la VETA Dakawa, Tarafa ya Dumila, Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro.

Ajali ya kwanza imetokea majira ya saa 11:30 jioni ya tarehe 30 Juni, 2016 ambapo watu 5 wamefariki dunia kufuatia malori mawili, mojawapo likiwa na shehena ya mafuta kugongana na kisha kuwaka moto, na ajali ya pili ikatokea hapohapo majira ya saa 10:00 alfajiri ya tarehe 01 Julai, 2016 baada ya basi la kampuni ya Otta High Class kuligonga lori la mafuta lililokuwa likiungua moto na kusababisha vifo vya watu 7 mpaka sasa.

Katika salamu zake kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe, Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshituko na masikitiko taarifa za vifo vya watu hao ambao licha ya taifa kupoteza nguvu kazi muhimu, ndugu, jamaa na marafiki wamepoteza watu waliowategemea na wapendwa wao.

“Ndugu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa wote waliopatwa na msiba na uwaambie naunga nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

“Pia nawaombea wawe na moyo wa uvumilivu na ustahimilivu na Mwenyezi awapumzishe marehemu wote mahali pema peponi, Amina”amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia amewaombea majeruhi wote waliolazwa hospitali na wale wanaoendelea kupata matibabu wakiwa majumbani, kupona haraka ili waendelee na kazi zao za kila siku.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
02 Julai, 2016
Share:

CHADEMA Waapa Kutibua Mkutano wa CCM .....Vijana 2000 Kupelekwa Dodoma Kwa Ajili ya Kazi Hiyo


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepanga kulisaidia Jeshi la Polisi kuzuia Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hivi karibuni Jeshi la Polisi lilitoa zuio la mikutano ya siasa ya wazi na ya ndani nchini kote, hata hivyo CCM imepanga kufanya Mkutano Mkuu tarehe 23 Julai mwaka huu mjini Dodoma.

Kwenye mkutano huo, Dk. Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM atakabidhi mamlaka hayo kwa Dk. John Magufuli ikiwa ni utaratibu wa kawaida wa chama hicho.

Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) limepanga kuzuia mkutano huo kwa madai ya kulisaidia Jeshi la Polisi kusimamia agizo lake kwa vyama vya siasa nchini.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Slaam viongozi wa Bavicha walisema, hatua hiyo ni katika kuhakikisha wanalisaidia jeshi kutekeleza amri iliyotolewa na Rais Magufuli ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa hadi mwaka 2020.

“Tumeandaa vijana takribani 2000 kutoka mikoa yote nchini watakaokwenda Dodoma kusaidiana na Jeshi la Polisi kutawanya mkutano usio halali wa CCM.  Kwa sababau Jeshi la Polisi limezuia mikutano yote ya siasa kwa sasa.

“Pia ni katika kuunga mkono kauli ya Rais Magufuli kwamba, hakuna mikutano ya vyama vya siasa mpaka mwaka 2020. Huu ndio msiamamo wa baraza.

“Mikutano yetu sisi kama Chadema tunazuiwa lakini CCM wanafanya. Mahafari ya chama cha mapinduzi yanafanyika. Ni jana CHASO (Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Chadema) Morogoro tumezuiwa lakini UVCCM (Umoja wa Vijana wa CCM) Mkoa wa Morogogo wamefanya na picha zipo. Hii sio haki, kama mbwai na iwe mbwai,”alisema Patrick ole Sosopi, Makamu Mwenyekiti wa baraza hilo.

George Tito, Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mbeya alisema “… ni kwamba, huko mikoani vijana wameshajipanga. Wana ari kubwa ya kwenda Dodoma.

“Tumeamua kufikia hatua hii kwa sababu tumekuwa tunaona hakuna haki katika nchi hii. Kuna mahafali yanafanyika vyuo vikuu, wenzetu CCM wanaruhusiwa sisi Chadema tunakatazwa.Vijana wa Chadema wamekuwa wakikamatwa bila sababu za msingi,” alisema Tito.
Share:

Friday, June 24, 2016

Mke Adai Kukimbiwa na Mumewe Kisa ‘Buku’ 3 Tu


SHINYANGA! Mama mmoja mkazi wa Kahama mkoani Shinyanga aliyejitambulisha kwa jina la Mwajei amedai kutelekezwa na mumewe (jina tunalihifadhi kwa sasa) kisa ‘buku’ tatu (3000) ya matibabu ya mtoto wao ambaye aligongwa na pikipiki.

Akizungumza kwa uchungu Mwajei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Juni 7 mwaka huu baada ya mtoto wao kugongwa na pikipiki kisha kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama ambapo kila alipomtafuta mumewe kwa ajili ya kumpa pesa ya matibabu hakueleweka.

“Mtoto aligongwa na pikipiki nikampeleka hospitali lakini kila nikimpigia mume wangu na kumuomba Sh. 3000 ya matibabu anasema kuwa kasafiri yuko Dodoma, mara yuko Singida, nateseka na huyu mtoto jamani,” alisema mama huyo.

Alipotafutwa mume wa Mwajei kwa njia ya simu, iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakujibu lolote.
Share:

Mtuhumiwa kesi ya Mwangosi akana Ungamo Lake Mahakamani


Mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Chanel Ten mkoani hapa, Daudi Mwangosi, Pacificus Simoni ametoa ushahidi wake mbele ya mahakama na kuieleza kuwa alilazimishwa kusaini ungamo mbele ya mlinzi wa amani bila kujua nini kilichoandikwa.

Alidai kuwa baada ya kutoka kuhojiwa kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) na Ofisa wa Makosa ya Jinai ya Mkoa (RCO), akifananishwa na picha ya gazeti la Mwananchi la Septemba 3, 2012 alipokana siyo yeye, alipelekwa kwenda kufanya ungamo kwa mlinzi wa amani, Frola Mhelela ambaye alikuwa shahidi namba tatu.

Alidai wakati anakwenda kwa mlinzi wa amani alisindikizwa na Staff Sajent Erick, ambaye alikuwa ameshika bahasha na kumkabidhi kwa mlinzi huyo.

Mtuhumiwa huyo alidai mlinzi huyo alitoa karatasi na kuisoma kisha baadaye alimuambia aisaini, naye bila kuhoji alisaini ile karatasi kwa sababu ilitoka kwa kiongozi wake ambaye ni RCO, Nyegesa Wankyo.

Katika kesi hiyo wakili wa utetezi, Rwezaura Kaijage aliiomba Mahakama kwamba mawakili wa upande wa Jamhuri wataleta majumuisho ya mwisho leo.

Hata hivyo, upande wa jamhuri ambao uliongozwa na wakili Sunday Hyera, ulisema hawana pingamizi lolote juu ya upande wa utetezi baada ya kukaa na kukubalina kwa pande zote mbili saa nane mchana watawasilisha majumuisho hayo.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Dk Paulo Kihwelo alisema Mahakama imekubali ombi la wakili wa utetezi kuleta majumuisho, huku Juni 27 wakisikiliza maoni ya wazee wa baraza kwa ajili ya kupanga hukumu
Share:

Friday, June 17, 2016

Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Manunuzi Wasomwa .....Waliohukumiwa kwa Rushwa Kunyimwa Zabuni, Mikataba yote Kuwa na Mashuhuda

MUSWADA wa Marekebisho ya Sheria ya Manunuzi wa Mwaka 2016, umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni jana na kuwekwa wazi kwa umma, na moja ya vifungu vinavyopendekezwa ni kuzuia mtu yeyote aliyewahi kuhukumiwa kwa rushwa, kufanya biashara na serikali.

Katika marekebisho hayo yanayopendekezwa na serikali, wizara, taasisi au shirika lolote la serikali wakati wa kufanya biashara na kampuni yoyote, ikibaini kampuni husika au mmoja wa wakurugenzi wake aliwahi kuhukumiwa kwa rushwa, biashara hiyo itasitishwa mara moja na taarifa kutolewa serikalini.

Mbali na watu waliohukumiwa kwa makosa ya rushwa, marekebisho hayo yamependekeza kuwa pamoja na sifa nyingine za viongozi wakuu wa serikali hasa maofisa watendaji wakuu, watapaswa kuwa na sifa ya ziada ya uzoefu katika masuala ya manunuzi.

Katika kukidhi haja ya kuondoa malalamiko ya sheria iliyopo kutumika kuibia nchi, marekebisho hayo yamesisitiza bei za huduma na bidhaa zitakazotolewa ziwe za soko, ununuzi ufanyike moja kwa moja kiwandani badala ya kupitia kwa mtu wa kati na mkataba wa manunuzi, lazima usainiwe mbele ya mashuhuda.

Watuhumiwa wa rushwa

Katika Ibara ya 83 ya Sheria hiyo, imependekezwa ibara ndogo ya pili kwamba shirika au wizara itakaporidhika kwamba kampuni au mtu anayependekezwa kupewa zabuni, amewahi kutangazwa na Mahakama kuwa alishiriki katika vitendo vya rushwa, ufisadi, au ukiukwaji wa taratibu wakati wa kushindania zabuni, ofisi hiyo ya umma itapaswa kukataa pendekezo la kumpa mhusika zabuni hiyo.

Ofisi hiyo ya umma, pia itapaswa kumtangaza mtu huyo au mzabuni ikiwa ni pamoja na wakurugenzi wake, kuwa hawapaswi kupewa zabuni yoyote inayogharimiwa na fedha za umma.

Pia ofisi hiyo ya umma, itapaswa kumtaka huyo mtu au mzabuni, kurejesha sehemu ya fedha aliyopewa kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa au huduma au kuzuia sehemu ya fedha iliyopaswa kwenda kwa mzabuni kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa au huduma.

Mapendekezo hayo yameendelea kuitaka ofisi husika ya umma ndani ya siku saba baada ya kutangaza kuwa mzabuni huyo, hafai kupewa zabuni inayogharimiwa na fedha za umma, kuwasilisha jina la mzabuni na wakurugenzi wake kwa mamlaka inayotajwa na sheria husika.

Mamlaka hiyo nayo imetakiwa na mapendekezo hayo ya sheria, kwamba baada ya kupata taarifa hiyo, kumfungia mtu au mzabuni husika asipate zabuni yoyote inayogharimiwa kwa fedha za umma, kwa muda usiopungua miaka 10.

Sifa za CEO

Katika mapendekezo kwenye Kifungu cha 23 cha Sheria hiyo, Kifungu Kidogo cha II, kimezungumzia uteuzi wa maofisa watendaji wakuu wa ofisi hizo za serikali.

Kifungu hicho kinaeleza kuwa ofisa mtendaji mkuu, atateuliwa kutoka kati ya wataalamu wenye uzoefu wa angalau miaka 10 katika fani za uhandisi, usanifu wa majengo, sheria, menejimenti ya ununuzi na usambazaji na ukadiriaji majengo.

Fani nyingine zilizotajwa ni pamoja na uongozi wa biashara, mipango ya kiuchumi na maendeleo au katika fani nyingine yoyote, lakini awe na uzoefu usio na shaka katika masuala ya ununuzi wa umma.

Bei ya soko

Katika Kifungu cha Tisa cha Sheria hiyo sehemu (o) imeitaka ofisi ya umma, wizara au taasisi ya umma, kila taasisi imetakiwa kuwa na taarifa ya bei ya soko ya bidhaa na huduma inayotumika mara kwa mara na ofisi husika kutoka katika ofisi husika ya umma ili kuhakikisha bei ya bidhaa na huduma zitakazonunuliwa, zinalingana na za soko.

Katika kuhakikisha ofisi za umma zinanunua bidhaa bora kwa bei ya soko, ununuzi wa umma umetakiwa kwa mujibu wa muswada huo, kufanyika kwa kuzingatia uaminifu wa hali ya juu, ushindani, uwajibikaji, kuzingatia kupunguza gharama, ufanisi, uwazi na kupata thamani ya fedha iliyotumika.

Aidha, ili kupata bei iliyo chini ya soko bila kuathiri ubora wa bidhaa au huduma, ofisi husika kwa nia ya kupata thamani ya fedha na ubora wa juu, imetakiwa kufanya ununuzi wa bidhaa na huduma mahususi moja kwa moja kutoka kwa mtengenezaji, au kiwandani, mwakilishi wa mtengenezaji au wa kiwanda, muuzaji wa jumla au mtoa huduma.

Wawekezaji wa ndani

Mapendekezo ya muswada huo, pia yametaka pale kampuni au taasisi ya umma inapolazimika kufanya ununuzi kutoka nje ya nchi, hasa kama ni suala la ushauri linafanywa na kampuni ya nje ya nchi, ofisi hiyo ya serikali inalazimika kuhakikisha kuna wataalamu wa ndani ya nchi.

Ushiriki huo wa wataalamu na kampuni za ndani katika shughuli za ushauri kutoka nje ya nchi, sheria hiyo imependekeza kuwa, kampuni yoyote ya ushauri ya nje ya nchi, inapoomba kazi katika kazi zinazogharimiwa na fedha za umma, lazima ishirikiane na kampuni, mshauri wa Kitanzania kwa asilimia mpaka 15.

Aidha, kampuni au mshauri huyo wa nje ili apewe zabuni katika shughuli ambazo zinagharimiwa na fedha za umma, kuna kigezo cha kuhakikisha wafanyakazi wa kampuni yake, zaidi ya asilimia 60 ni Watanzania.

Mbali na kuwa na asilimia 60 ya wafanyakazi Watanzania, kampuni husika lazima ieleze kiwango cha bidhaa na huduma zinazozalishwa ndani ya nchi, ambazo itazinunua katika utekelezaji wa shughuli zake.

Muswada huo unatarajiwa kujadiliwa na kupitishwa katika Bunge hili, ili kuzuia matumizi mabaya ya fedha za umma, ambazo katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2016/2017, asilimia 40 ya trilioni 29.53, imepelekwa katika miradi ya maendeleo.
Share:

Uenyekiti wa Rais Magufuli CCM Waiva......Kamati Kuu ya Chama Hicho Kukutana Dar es Salaam Kesho

Maandalizi ya CCM kumkabidhi Rais John Magufuli uenyekiti wa chama hicho ili ashike kofia zote mbili, yataanza kesho katika kikao cha Kamati Kuu kilichopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam.

Taarifa kuhusu kikao hicho iliyotiwa saini na msemaji wa chama hicho, Christopher ole Sendeka ilisema: “Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM itafanya  kikao cha kawaida siku ya Jumamosi jijini Dar es Salaam. Kikao hicho kitafanyika chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais mstaafu Jakaya Kikwete.”

Japokuwa taarifa hiyo haikueleza ajenda za kikao, habari kutoka ndani ya chama zinasema kikao hicho cha siku moja kinatarajiwa kujadili masuala mbalimbali, ukiwamo mchakato wa makabidhiano ya kiti hicho katika mkutano mkuu wa chama hicho utakaofanyika mwezi ujao.

Kipindi cha uongozi wa chama kwa Kikwete kitamalizika mwakani, lakini imekuwapo desturi kwa rais mpya kuachiwa kofia hiyo mapema, hivyo Rais Magufuli anatarajiwa kurithi mikoba ya uenyekiti mwezi ujao.

Vilevile, kikao hicho kinatarajiwa kuhitimisha hoja zinazodaiwa kuibuka katika vikao vya ndani vya chama hicho kwamba CCM inataka kuvuruga utaratibu uliodumu kwa muda mrefu wa mwenyekiti kumwachia kijiti Rais aliyeko madarakani.

Madai kuhusu mkakati huo wa ndani yalisambazwa katika mitandao ya kijamii yakimnukuu Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, lakini Ole Sendeka alisema hana sababu yoyote ya kumjibu kiongozi wa dini.

Februari 5, mwaka huu Kikwete alipokuwa anazungumza na wazee wa Manispaa ya Singida alisema sherehe za mwaka huu za maadhimisho ya miaka 39 tangu chama hicho kuanzishwa zilikuwa za mwisho kwake akiwa mwenyekiti, kauli ambayo iliashiria ataachia mapema uenyekiti.

Kwa desturi, wenyeviti wa CCM huwa wanaachia madaraka yao kabla ya muda wa uongozi wao kumalizika.

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alikabidhiwa chama na Alhaji Ali Hassan Mwinyi mwaka 1996 badala ya 1997 na Mkapa alimkabidhi Kikwete kiti hicho mwaka 2006 badala ya 2007.

Kulingana na kalenda ya chama hicho, Mkutano Mkuu wa CCM kumchagua mwenyekiti unapaswa kufanyika mwaka 2017, lakini utafanyika mwaka huu kuendeleza utamaduni wa kung’atuka mapema.

Habari kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa kinachoendelea sasa mikoani na wilayani ni maandalizi ya mkutano huo mkuu yanayosimamiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Bara, Rajabu Luhwavi kwa niaba ya Sekretarieti.

“Kikao hicho cha Kamati Kuu ndicho kitakachojadili ajenda za mkutano huo sambamba na kupanga tarehe ya kufanyika kwa mkutano mkuu,” zilieleza taarifa hizo.

Dk Magufuli anatajwa kuwa uongozi wake ndani ya CCM utakuwa wa kasi ya aina yake kutokana na hatua mbalimbali za ‘utumbuaji majipu’ anazozifanya ndani ya Serikali tangu Novemba 5, alipoapishwa kuwa Rais.
Share:

Tanzania Kuanza Kutumia Kiswahili Katika Mikutano Yote ya Kimataifa

TANZANIA inatarajiwa kuanza kutumia Kiswahili katika mikutano yote ya kimataifa itakayowakilishwa na viongozi wake baada ya serikali kukamilisha kutuma wataalamu watakaotafsiri lugha hiyo kwa watumiaji wa lugha nyingine duniani.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hayo jana katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Zainabu Vulu (CCM).

Vulu katika swali lake alihoji namna serikali inavyoenzi lugha ya Kiswahili ambayo ilitumika na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuunganisha Taifa na inatumiaje fursa ya kutumika kwa lugha hiyo kimataifa, kuwa ajira kwa Watanzania.

Akifafanua jibu lake, Majaliwa alisema tayari serikali ilishaamua Kiswahili kuwa lugha rasmi ya kutumika serikalini na hata bungeni na sasa lugha hiyo imekua zaidi na kuwa moja ya lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kwa mujibu wa Majaliwa, tayari duniani kote vyuo vikuu vimeanza kufundisha Kiswahili, hali iliyosababisha kuongezeka kwa mahitaji ya walimu wa kufundisha lugha hiyo kutoka Tanzania.

Kutokana na uhitaji huo, Majaliwa alisema vyuo vikuu karibu vyote nchini, vinafundisha walimu wa lugha hiyo kwa ajili ya kukidhi mahitaji hayo ya kimataifa, lakini pia serikali inajiandaa kupeleka wataalamu wa kutafsiri Kiswahili kwenda katika nchi mbalimbali.

Alisema lengo la serikali kupeleka wataalamu hao katika nchi mbalimbali ni kuwezesha viongozi kutoka Tanzania wanapokwenda katika mikutano ya kimataifa, watumie Kiswahili na wataalamu hao watoe tafsiri kwenda kwenye lugha nyingine za kimataifa.

Alisema kwa sasa Tanzania imeshapeleka walimu wa lugha hiyo Burundi, Rwanda, Uingereza na Ufaransa ambako wanafundisha lugha hiyo na kati ya lugha kubwa za kimataifa, Kiswahili kama si lugha ya sita ni ya nane.

Naye Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima (CCM), alimtaka Waziri Mkuu kuangalia uwezekano wa kuruhusu wabunge kuwa wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama za wilaya na mikoa.

Akijibu ombi hilo, alisema wajumbe wa kamati hizo katika wilaya, mikoa na kitaifa, wameainishwa na Sheria ya Usalama wa Taifa kuwa ni wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, ambao ni tofauti na mbunge ambaye ni mwakilishi wa wananchi kisiasa.

Alisema majukumu yao ni kuangalia hali ya usalama kwa undani, lakini sheria hiyo haijamzuia mbunge au mwananchi yeyote, kwenda kutoa taarifa kama ilivyotokea katika mauaji ya hivri karibuni, ambapo kamati hizo kutokana na ushirikiano kutoka kwa wananchi, wahusika wameanza kukamatwa mmoja baada ya mwingine.
Share:

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger